Ahadi 10 za TANU, matapishi?
Na Amos Nyaigoti (TUDARCo)
Historia nzuri tulizozipata maishani ni miongoni mwa vitu ambavyo watu huwa tunajivunia, kwani hupamba maisha yetu na kuandaa taswira kwa maisha yajayo.
Mnamo mwaka 1962 Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere akiwa muasisi wa TANU akizidi kukiimarisha Chama chake aliamua kuweka ahadi kumi ili kila mwanachama wa TANU aweze kuahidi.
Ahadi zilizokuwa kama kiapo kwa wanachama hao katika kutekeleza malengo ya TANU kwa mustakabali wa chama na Taifa letu la Tanzania ambapo wakati huo lilijulikana kama Tanganyika.
Mwl. Nyerere aliweka ahadi kumi ambazo kiuhakika katika Taifa hili zimepuuzwa kama kaniki yenye viroboto na kufubaa.
Nitaanzia ahadi ya mwisho kuja ya kwanza, kadiri walivyoziahidi kama njia ya kuonyesha utayari wa kuwa mwaminifu na mtii kwa chama na Taifa,
Ahadi ya kumi, na ahadi ya tisa ni juu ya utii, uaminifu na uadilifu. Ambapo ahadi ya kumi ilisema “Nitakuwa mtiifu kwa Rais wa Tanganyika (Tanzania)” Ahadi ya tisa “Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika”
Sasa je uadilifu ni pamoja na kutuhumiwa kulifilisi taifa? Ni pamoja na kujilimbikizia shehena ya hazina ya wananchi? Cha kuvutia na kupendeza machoni na masikioni mwa wAuhumiwa wizi wa hazina wanathubutu kuitwa wachapakazi hodari, waaminifu na waadilifu. Uraia mwema ulionuiwa na Tanu uko wapi?
Ama kujilimbikizia mali, kufanya biashara za dili huku taifa likiangamia ndio uraia mwema? Ikiwa watu wangekuwa raia wema, waaminifu na waadilifu misamiati ya ufisadi, uchakachuaji ingetoka wapi?
Ahadi ya nane inasema ‘Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko’ katika ahadi hii ndipo wengi wamechemsha na kudhihirisha matapishi yao juu ya misingi ya waasisi wao.
Kwa viongozi wetu imekuwa hivi “ukweli kwangu mwiko nitakuwa mfitini daima” hili linadhihirishwa na ahadi wanazotoa hawazitekelezi, sambamba na hiyo ni sababu gani zinawafanya kulipana pesa kifisadi? Richmond na Dowans…na mengine mengi ambayo hadi kesho hakuna raia ambaye anaujua ukweli.
Ahadi ya saba “Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu” hakika kila kitu kifanywacho katika taifa lolote lile ni kuijenga nchi. Ushirikiano ni kitu chema katika kulijenga taifa,
Ndio maana hata viongozi wetu walipokuwa katika harakati za kuusaka uhuru waliweza kuwa na kauli mbiu za kuuganisha watu wote ili kuimarisha ushirikiano, kwa mfano Tanzania tulisema ‘Uhuru na Umoja’ Kenya wakawa na ‘Harambee’n.k.
Ikiwa ushirikiano ndio msingi imara katika kulijenga taifa lolote, inakuwaje baadhi ya…. Wamejaaa umimi kuanzia sera zao hadi muonekano wao. Hapa wanasiasa wote wanahusika, baadhi yao hupinga kila jambo lisemwalo ilihali limesemwa na mwanasiasa asiye wa chama chake. Huu ni upuuzi!
“Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote” hii ni ahadi ya sita iliyoelekeza kila msomi kutumia elimu kwa faida ya taifa lake. Lakini wasomi wa nchi yetu wanaitunia elimu kupiga picha na mali zetu wakiwacheka wenzao kwa kusema “mulikuwa wapi kusoma enyi watu wajinga?
Tumekuwa wabinafsi, dhamana tunazopewa kwa sababu ya visomo vyetu imekuwa tiketi ya kuwanyonya wanyonge, tumepuuza yote ambayo yalielekezwa na waasisi wa nchi yetu ambao walishirikiana na wasio soma kulikomboa taifa hili na wakafanikiwa.
Ahadi ya tano ilisema “Cheo ni dhamana sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu” leo ukimwambie mtu kula kiapo kuwa hatakitumia cheo chake kwa manufaa yake mtamalizana.
Hapo sitaki kuandika mengi maana naweza kutukana, hivi dhamana ya uongozi iko wapi, kama viongozi wamekuwa kero kwa raia wao? Wamekuwa manyapala kwa watu waliowachagua…. Wapo baadhi hudiriki hata kujitenga na wanaowaongoza, huo ni ufujifu wa vyeo na inastahili waadhibiwe.
Ahadi ya nne “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala sitatoa rushwa” haya ndio matapishi mazito kuliko yote. Hapa ni vigumu kuwasema wala rushwa maana kila mtu Anadai kuichukia rushwa huku ikizidi kushamili, sasa sijui nani msaliti tumsomee albadili.
Tukisoma ahadi ya tatu ilisomeka “Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umasikini, ujinga, magonjwa na dhuluma” Bila kusahau mwalimu Nyerere akiongoza nchi mara baada ya uhuru alitangaza vita dhidi ya maadui watatu wakuu: Umasikini, maradhi (magonjwa) na ujinga.
Miaka 49 ya Uhuru wa Tanganyika yote haya huwa tukiyasikia kama wimbo wenye ala nzuri yenye ujumbe usiotekelezeka ama kutoeleweka kabisa.
Hosipitali wauguzi wanawatusi na kuwaadhibu wagonjwa, nadhani vita dhidi ya maradhi maana yake kupigana na wagonjwa.
Viongozi wetu na baadhi ya watu wenye mafanikio, wanawatenga masikini hii ndio maana ya vita dhidi ya umasikini maana hakuna apendae umasikini.
Kudhulumu haki na mali za raia mchana kweupe na mengineyo lukuki yote hayo yanaendeleza vita dhidi ya maadui wtatu wa Tanzania? Aksanteni sana.
Yaani ujinga mtupu, kama sivyo ni kwa nini viwanda na mashamba vilivyokuwepo vife? hakika ni masikitiko kwa wana wa nchi. Kuhusu umasikini kila kukicha ni afadhali ya jana umasikini wa kipato uazidi kuporomoka.
Dhana ya kuwa ‘nitajitolea nafsi yangu kuondoa umasikini’ yafaa iwe ‘nitajitolea nafsi yangu kuongeza umasikini’ kwa kuwa mipango inayopangwa mwaka hadi mwaka imegeuka na kuwa majuto kwa wana na binti wa nchi hii.
Wale masikini watoto wasiosoma wakirandaranda mitaani ikiwa hakuna mipango ya kuwafanikisha hawa ni kina nani watakuwa wataalamu wa kesho? Ama tuendelee na kauli zile za vijana taifa la kesho? Haihai ni lazima urejesho ufanywe ujinga uondoke.
Kuhusiana na magonjwa sina haja ya kueleza, kwani inanikumbusha jinsi kina mama, watoto na watu masikini wanavyoteseka na kufa kwa kukosa matibabu. Wauguzi wana roho mbaya kias cha wagonjwa wengine kufa baada ya sura zenu zisizoficha ushetani wenu kwao na roho zenu.
Inanikumbusha pia wana wa nchi wanavyolazwa sakafuni kwa kukosa vitanda huku raslimali za nchi zikifaidiwa na watu wachache, wanaojifanya Watanzania na kufanya wengine ‘wadanganyika’
Miaka 49 ya uhuru vijijini kina mama wakitembea zaidi ya kilometa 5 kwenda kupima watoto uzito, achilia mbali matibabu wanaokwenda mpaka kilometa 10, eti miaka 49 ya uhuru ikisindikizwa na mizinga 21 kila mwaka.
Katika ahadi ya pili ilisomeka “Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote” sasa kama kawaida tusaidiane kutafakari ni utumishi gani ulionao wewe kiongozi? Na hapa sio kiongozi wa nchi tu hata ninyi viongozi wa familia msije kaa mkidhani hamuhusiki, nanyi wapuuzi kama mmekubali familia zenu zikiteketea huku ninyi mkiivinjari na pato lenu.
“Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja” hivyo ndivyo ahadi namba moja ilivyosema.
Ingali twasema wanadamu wote ni sawa lakini si kweli, ndio maana kuna manyangumi wasiojua kuwa kuna kundi kubwa la walala hoi wanahitaji tunda la uhuru wamezidi kujishibisha matumbo yao,
Hawa si wengine bali ni makaburu, ni wakoloni weusi walioamua kuwasaliti wenzao na kujiona na haki zaidi, wanakula kuku kwa mrija, wanatibiwa majuu, wa wana wao visomo vyao ni vya kuruka mipaka,
Kwa sababu usawa wana TANU waliousema kwao ni matapishi, ni kitu ambacho hawatakirudia kamwe, watoto wao kusoma shule za ‘saint. Kayumba’ ni fedhea kwa sababu shule hizo ni za wana TANU na walalahoi wengine wasioshiriki utandawazi.
Ahadi kumi za TANU misingi ya taifa ambalo viongozi na raia wake wamezisaliti, wakipiga mayowe ya maendeleo. Hakuna nchi duniani imeendelea huku ikisau misingi na ahadi za uangavu wa nchi. Acheni upuuzi wa kupamba nyumba huku msingi ukiporomoka.
Mawasiliano ya mwandishi wa makala hii
0762 382005
nnyaigoti@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment