Kutoka Jamii Forum...
MEYA wa Jiji la Dar es Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT), Dk Didas Masaburi, amewataka wabunge wa Jiji la Dar es Salaam kumwacha akague miradi na viwanja vya Jiji hilo, baada ya ukaguzi na taarifa kutoka, ndipo wananchi watajua nani wa kuachia ngazi.Amesema baada ya ukaguzi wa miradi hiyo ambayo miongoni mwao inawagusa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu na Mbunge wa Ilala Mussa Hassan Zungu ambayo waliingia mikataba aliyodai haieleweki, ndipo ukweli utajulikana.
Amesema, kutokana na mikataba hiyo, ndiyo maana wanajitahidi kumnyamazisha ili asiendelee kukagua miradi na kuibua uozo uliochangia Jiji kukosa mapato.
Masaburi alitoa kauli hiyo jana mjini hapa kwenye mkutano wa jumuiya za Serikali za Mitaa uliokutanisha viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, ambao unafanyika kwa siku mbili ukiwa na lengo la kupitisha Bajeti ya mwaka huu, uchaguzi wa viongozi na kupitia taarifa za utendaji wa mwaka jana.
Alisema ,lengo la baadhi ya wabunge hususan wa Jiji la Dar es Salaam kumtaka ajiuzulu kutokana na kashfa aliyoiibua ya uuzwaji wa mali za Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), ni kumfanya asitimize ukaguzi wa mali za Jiji na kuwasihi wabunge hao waache kutafuta umaarufu kwani baadhi yao ni miongoni mwa watakaoumbuka kutokana na kuuza viwanja na mali zingine za Jiji .
Alisema suala hilo limeibuliwa na baadhi ya wabunge kwa aina tatu; moja ni kujipatia umaarufu, pili, wasioelewa kutojua ukweli na kuropoka na wengine kuujua ukweli ila wanaropoka kutafuta umaarufu wa kisiasa na kundi lingine linataka sifa na kuonekana kuwa ni mashujaa wa kupiga vita ufisadi.
Alisema, amefanya ukaguzi wa mali za Jiji lakini amegundua ubadhirifu wa mali katika Uda na alipofuatilia kwa makini, aligundua kuwa ulitokea akiwa hajachaguliwa kuwa Meya na ulianza mwaka 2008 wakiwamo baadhi ya wabunge wanaopigia debe suala hilo.
Alisema, alipochaguliwa kuwa Meya alikuta tayari watu wamesaini mkataba wa kuuza hisa za Uda na yeye alihoji mali za Jiji ziliko huku likiwa na mali nyingi lakini halina mapato na alipopitia mikataba akabaini ubadhirifu huo Uda na alipomwuliza Mkurugenzi wa Jiji mali wazouza ziko wapi na Mei 5 akamwuliza Mwenyekiti wa Bodi Idd Simba, akaambiwa zilishauzwa na alipoendelea kumhoji Simba akasema anadhani Mkurugenzi wa Jiji aliwaeleza uuzwaji wa Uda.
Alisema, UDA imeuzwa kwa kampuni ya Simon Group Limited kwa Sh milioni 285 na walipokaa kwenye kikao alimuuliza Mhasibu akasema Sh milioni 200 hazipo zilizobaki ni Sh milioni 85 hivyo kuchukua jukumu la kuvunja Bodi na kumsimamisha kazi Mkuu wa Idara na kumteua Kaimu Mtendaji kwa muda, ili uchunguzi zaidi wa suala hilo uendelee.
"Hawa watu wanapiga kelele kupata umaarufu lakini nawaambia hususan wabunge wa Dar es Salaam, wakae chonjo, maana hivi sasa naacha kazi za Jiji nashughulika na mikataba waliyoingia juu ya mali za Jiji, Majengo ya Machinga Complex, soko la Kariakoo, Chibuku, nk.
“Wasipate umaarufu kwa kutumia midomo, majibu watayapata na baada ya ukaguzi huo ndipo nitajiuzulu, lakini hivi sasa wanataka ninyamazishwe ili mambo mengi waliyoyafanya yasijulikane, na mimi nawaambia nitawaumbua mmoja baada ya mwingine, hapo ndipo wananchi watajua kama nimeiba au la," alitamba.
Alimtaka Mtevu akae chonjo kwani mikataba aliyoingia DDC na Zungu katika uwekaji wa nyavu jengo la Machinga Complex uliogharimu Sh bilioni 2 unawahusu ikiwamo mikataba ya viwanja vya Jiji.
Juzi wabunge wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mtemvu (Temeke-CCM) walizungumza na waandishi wa habari Dodoma na kueleza kusikitishwa na tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni, taratibu na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa UDA.
Wabunge wa Dar es Salaam ni Mtemvu, John Mnyika (Ubungo), Zungu (Ilala), Dk. Faustine Ndungulile (Kigamboni), Idd Azzan (Kinondoni), Eugen Mwaiposa (Ukonga), Halima Mdee (Kawe), Dk. Makongoro Mahanga (Segerea) na wengine wa viti maalumu Philipa Mturano, Mariam Kisangi, Zarina Madabida, Angellah Kairuki na Fanella Mkangara.
Wabunge hao walitaka Massaburi, Mkurugenzi wa Jiji Bakari Kingobi na watendaji wote wa Jiji la Dar es Salaam wasimamishwe mara moja katika kipindi chote cha uchunguzi na kuchukuliwa hatua stahili baada ya uchunguzi huo kwa mujibu wa sheria, kanuni na maslahi ya umma.
Chanzo cha Habari: Habari Leo na Jamii forum
0 comments:
Post a Comment