Tanzania makini ya watu makini Msilete Dharaooo



Tanzania ni miongoni  mwa nchi makini duniani ambayo ina mengi ya kujivunia japo kila uchao tunasikia watu wakilalama na hata kutoa maneno machafu, kejeli na hata wengine hutoa maneno ya laana wakidai bora wazaliwe mbwa ulaya kuliko kuzaliwa mtanzania.

Jambo la kusikitisha ni kuwa miongoni wa wabezaji wa nchi yetu ni wasomi na wanafahamu fika kuwa jamii inawaamini kuwa wao ndio dira ya taifa letu lakini kwa maneno na vitendo vyao vinathibitisha kuwa watu hao ni wasomi mbumbumbu masikini wa fikra ambao kama kungekuwa na sheria za kuwawajibisha kwa maneno na watendayo basi wengi wao wangehukumiwa vifo ama kwa sheria za zamani kupigwa mawe hadi kufa.

Wapo baadhi ya watu wanadiriki kusema eti Tanzania imelaaniwa na ndio maana masikini watazidi kusikinika na matajiri watazidi kutajirika na wanakamilisha kauli zao kwa kudai kuwa hata siku moja haki haitapatikana mpaka Mwisho wa dunia.

Maneno hayo yanatolewa hadharani huku maendeleo ya habari zikiwemo simu za mikononi, mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari vikikuza mabezo na kutia uzito zaidi ya vile yalivyotolewa katika vinywa vya wasemaji.

Kwa wale wote wanaolaani nchi yetu kwa kutokujua ama kwa kuwafuata washereheshaji wa jamii wanapaswa kujua kuwa Tanzania ni nchi ya asali na maziwa ambayo katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru imedumu katika misingi ya utu, uvumilivu na nakutokukubali machafuko ya aina yoyote jambo ambalo limayafanya makabila zaidi ya 120 kuonekana kitu kimoja.

Ni fahari kujiita mtanzania japo baadhi ya watani husema ukienda nje usiseme umetoka Tanzania bali sema nimetoka katika ile nchi iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyere ambaye ni Rais wa kwanza wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na hili linadhihirisha kukubaliana na misingi ya utu ya waasisi wetu ambayo iliwafanya wajulikane hata katika mataifa mengine.

Kutokana na matukio  kadha wa kadha yaliyotokea na yanayoendelea kuonekana yakiwemo rushwa, uvunjivu wa sheria, elimu duni, watoto wa mitaani, ukosefu wa ajira, mikataba mibovu, mauaji ya walemavu na mengineyo lukuki  yanaifanya Tanzania kuwa si mahali salama  pa kuishi, hapana! bado tuna nafasi ya kuifanya na kuiendeleza kuwa pahala salama kwa watu wote kwani vyovyote ilivyo hii ni nchi yetu htuwezi kuikimbia.

Upo usemi usemao dawa ya tatizo sio kulikimbia bali ni kulitaftia ufumbuzi katika njia inayofaa hata nyumba yako ikiwa na matatizo hauikimbii bali unatafuta namna ya kuyamaliza matatizo hayo ili kuifanya kuwa salama kwako na kwa wahusika katika familia hiyo wakiwemo ndugu jamaa na marafiki kama ambavyo tunajua watanzania sote ni ndugu hata kama hatukuzaliwa kwa damu moja.

Kwa wale  wasiojua nchi yetu ni ya aina gani basi wajue kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza duniani kwa amani na utulivu ambao unatufanya kuishi na wageni wa kila aina, kwa amani na ushirikiano japo wengi wao sio waaminifu kwetu kama ambavyo tunawaamini.

Nchi hii ambayo ni mhimili na mfano wa kuigwa Afrika Mashariki na katika mataifa mengine ni ya tatu Afrika kwa utajiri wa madini, ya tatu kwa uwingi wa mifugo idadi kubwa ikiwa ni ng’ombe, na ni nchi ya pili Afrika baada ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo  kwa utajiri wa misitu na mito mingi isiyokauka.

Tanzania ina hekta 29 millioni ya ardhi bora yenye rutuba kwaajili ya kuzalisha mazao mbalimbali ya biashara lakini kubwa ni uzalishaji wa mazao ya chakula kwa binadamu na mifugo japo wapo wenzetu wanakabiliwa na njaa kwa uzembe na uvivu wa baadhi ya wanajamii wakiwemo viongozi wetu ambao wameshindwa kuendeleza kilimo kwa vitendo japo wamepiga hatua kidogo.

Nchi hii yenye watu takribani milioni 42 ni ya kwanza duniani yenye asilimia 18 ya maji yote baridi yanayofaa kwa matumizi ya binadamu, matumizi ya viwanda na matumizi ya kilimo japo bado kilimo chetu bado kinategemea mvua kwa asilimia kubwa.

Katika sekta ya utalii Tanzania ni ya pili kwa vivutio vya asili vya watalii baada ya Afrika ya kusini, kuna urithi pekee wa dunia kama mlima Kilimanjaro, Ngorongoro crater, lake Ngosi-Mbeya, milima ya udzungwa, Rungwe, Meru na pia kuna mbuga za wanayama zenye wanyama wa kila aina ikiwemo Serengeti ambayo ni kubwa zaidi duniani.

Fukwe za bahari na maziwa zilizopo Tanzania ni bora ambazo sio tu ni kuvutio kwa watalii bali ni zawadi tosha kwa raia wote japo wawekezaji wengi wamezimiliki ili kulipatia taifa mapato kwa kuzifanyia biashara kwa baadhi ya wageni na watanzania wenye kumudu gharama za kuvinjari.

Kwa upande wa nishati humu humu nchini kuna makaa ya mawe kwa wingi yanayopatikana kiwira na Mchuchuma , kuna gesi ya songosongo na kipekee zaidi Tanzania inazalisha madini yenye jina linalotokana na jina la jamhuri ya muungano yaani “Tanzanite” lakini kwa bahati mbaya madini hayo huuzwa nje ya nchi katika soko la kimataifa kwa chapa za  Afrika ya kusini India na Kenya.

Tanzania hii inayobezwa na baadhi ya wasio na mapenzi mema kwa raia wema inamiliki asilimia 46 ya ziwa kubwa Afrika na la pili duniani ambalo ni ziwa Victoria lenye samaki wa kutosha kuilisha kanda ya ziwa yote japo baadhi ya watu wanahujumu ziwa hilo kwa uvuvi haramu na kulichafua kila uchao.

Bandari nyingi zinazopatikana hapa kwetu zina vina virefu sana kwa mahitaji ya bandari za kimataifa kama bandari ya Mtwara, Dar es salaam, na Tanga lakini kutokana na wahujumu uchumi wachache ambao ni mabepari weusi kwa kushirikiana na mabepari weupe wamesababisha bandari kupoteza sifa zake za kuhudumia nchi nyingi za Kiafrika zisizozungukwa na bahari.

Tanzania ina mikoa zaidi ya 25 ambayo imegawavyia katika majimbo zaidi ya 200 ya uchaguzi ambayo yanaongozwa kwa kufuata mfumo wa vyama vingi unaokubalika kimataifa kuwa ni msingi wa demokrasia.

Yote hayo yanadhihirisha kuwa Tanzania ni ya watu makini na hatupaswi kujidharau wenyewe kwa kuangalia mapungufu na changamoto zilizopo bali tujitathmini upya na kuamua kwa dhati kabisa kuiboresha kwa kusimamia amani na raslimali zetu ili zitufaidishe sote.

Wakati tukiadhimisha  miaka 50 ya uhuru ni vema wananchi wote tushirikiane kumkemea yeyote anayebeza amani na utulivu wetu, tuwapinge wote wanaotufanya tudhalilike na hata kuitwa eti wadanganyika na si watanzania, tusimame imara kutetea raslimali zetu na tusikubali kamwe kugawanyika kwa misingi ya ukabila, ukanda, udini na asili zetu daima tusimamie haki, usawa na kupambana na maadui watatu wa maendeleo yaani maradhi, umasikini na ujinga.

0 comments:

Post a Comment