Ualimu, kufeli, kufaulu na Taaluma...upuuzi mtupu.


Utaratibu wa wanafunzi ambao hawakupata alama za kutosha kuendelea na masomo ya juu kujiunga vyuo vya ualimu nadhani ulikuwa unafaa sana kwa taifa ambalo lilihitaji watu wasio na elimu ya kutosha kuletea upinzani katika mfumo wa uongozi na pia shughuli nyingine za maendeleo.

Utaratibu ambao umedumu kwa muda mrefu nchini kwetu umekuwa ukitekeleza sera za mataifa fulani kipindi cha ukoloni ambayo yalikuwa na mlengo wa kuwaandaa waafrika kuwa watumwa wa fikra za watu fulani wenye maslahi binafsi.

Kwa waalimu waliofeli kujiunga na elimu ya juu na kuwa walimu wa kuwaaandaa wasomi kwaajili ya kulikwamua taifa katika umasikini na kuendeleza kizazi nadhani wakuu wetu wa masuala ya elimu walichemka kidogo.

Ni ukweli usiopingika kuwa mwanafunzi anaweza kumzidi mwalimu wake, na ndio maana tunaona wanafunzi wengi wamekuwa mawaziri ama maraisi na kupokea mshahara wa mara hadi elfu kumi ya walimu waliowafundisha. Lakini hata siku moja kumzidi mwalimu wako haimaanishi wewe ni bora kuliko mwalimu aliyekufundisha..mwalimu ni mwalimu tu, kwa kuwa alikufuta ujinga na kukufanya ufike pale ulipo sasa.

Swali, je? kama mwalimu aliyekufundisha alikuwa mwalimu kwakuwa alifeli, je wewe unayemzidi unamzidi kwa elimu ya kufeli, unmzidi upuuzi ama unamzidi maarifa ya kufeli?

Ni imani kuwa walimu walitakiwa kuwa wasomi wakuu ambao wamefaulu kwa alama za juu kuliko kawaida. ili watakaowazidi walimu wajisifu kwa kuwazidi taaluma.

 Labda kwakuwa watawala wetu wa zamani walikuwa wanaogopa kukosolewa , na wengi wao walikuwa hawana elimu ya kutosha ya uongozi, walikuwa wanaongoza kwa kutumia uzoefu tu ama kwa umri waliokuwa nao uliwasaidia kuonekana wana busara za kuongoza, ndio sababu ya kuwekas vigezo vya kufeli kama ngazi ya kuwa mwalimu.

Kwahivyo waliokuwa wanapanga utaratibu wa kujiunga na vyuo vya ualimu walikuwa na sera za kikoloni vichwani mwao. kwanini walikubali wanafunzi walipopata alama za chini katika mitihani wajiunge na vyuo kwaajili ya kuwaandaa wanafunzi ambao watakuwa kizazi makini cha kulikomboa taifa hapo baadaye?

Lakini kwa upande mwingine labda tujiaminishe mfumo wa kutumia alama zinazopatikana katika mitihani ni kigezo cha kipuuzi tu. Kwani mwanafunzi anaweza kuwa na akili za kutosha na makini kuzishughulisha akili hizo, lakini siku ya mitihani akawa ana mambo mengi yatakayo mchanganya akashindwa kujibu maswali ipasavyo, na hapo ndipo anahesabiwa amefeli kabisa katika elimu, ambapo wengine ndo huamua kujiunga na ualimu ama wengine kwenda kukaa nyumbani wakisubiri kuanzisha familia.

Kwa wale ambao wanahesabika kuwa wamefeli, kujiunga ualimu wameleta mabadiliko makubwa sana nchini kwetu kwakuwa, hakuna taaluma ambayo ina umuhimu kuliko ualimu, lakini vilevile kwa nyakati hizi, hakuna taaluma amabayo baadhi ya washenzi wanaidharau kama ualimu.

Tunawaita washenzi bila aibu wanaoidharau taaluma ya ualimu,kwakuwa walimu ambao wanasemekana walifeli mitihani yao, huenda ndio waliofulu kuliko wanafunzi wowote katika mashule ya hapa nchini.

Hilo linajidhihirisha kwa haya yafuatayo...elimu ya hapa nchini wengi ambao hufaulu sio kuwa wana akili sana hapana. Wengi hufaulu kwakuwa wanajua kukariri kile kinachosemwa ama kufundishwa na walimu wao.

Wengi wanaohesabika kuwa wanafeli inawezekana ndio watanzania halisi, kwakuwa watanzania halisi wengi wanapimwa umakini wao kwa vigezo vya kishenzi... na kushindwa kuvipata vigezo hivyo. Huwezi kumpima mwanafunzi akili kwa kumpatia mtihani pekee wa masaa matatu kwa mambo ambayo ameyasoma kwa miaka zaidi ya kumi na mbili.

Kwani hakuna vigezo vingine vya kupima uelewa wa mwanafunzi? walimu wengi wa nchi yetu wanasemekana walifeli, lakini si kweli hata kidogo...huwezi kumpima mtu kwa mitihani ya kipuuzi eti ukashusha hadhi yake kuwa hana akili.

Utata uliopo nchini ni kuwa wengi wanaoenda ualimu wanasema hivi wakiwa shueleni" mimi nikifeli nikashindwa kuendelea na elimu ya juu nitajiunga ualimu"

Hilo ni kosa kubwa, kwani kufeli hatua moja haimaanishi ni kigezo cha kwenda hatua nyingine. bali kufeli hatua moja no changamoto unapoelekea hatua nyingine.

Na kubwa ni kuwa kupata alama ndogo katika mitihani pekee haimaanishi kuwa umefeli. unaweza kufeli mitihani lakini una akili kuzidi wale wote wanaofaulu. 

Yaani watu wachache walikaa na kuamua kuwa alama za chini ndio kigezo cha kujiunga ualimu. Kumbe basi, matatizo yapo katika waandaa utaratibu wa taasisi zetu za elimu na sio kwa wanafunzi kufeli ama kufaulu.

Kosa kubwa kwao ni kuwapima wanafunzi kwa mitihani.....na kosa lingine kubwa ni kuwaaminisha watu kuwa wanaostahili kwenda ualimu wawe na lama fulani hadi fulani...huku alama hizo zikiwa za chini.

Vema basi, utaratibu wa elimu ukawa hiviii : elimu ya juu katika taasisi zote, vigezo vikawa sawa, walimu wasipimwe kwa mitihani pekee...bali watumie vigezo vingine mbalimabali...na wanafunzi waamue kusomea taaluma fulani amabayo ipo mioyoni mwao.

Huenda kwakuwa waliondaa mitaala ya kujiunga na vyuo vya ualimu nao walifundishwa na walimu waliofundishwa na walimu walioamua kwenda ualimu baada ya kupata alama ndogo na kushindwa kuendelea na elimu zaidi na kuamua kuwa walimu kwakuwa tu hawaakuwa na pahala pengine pa kukimbilia wakaamua kujiokoa kwa kuwa walimu ndio maana elimu ya tanzania mara kadhaa tunailaani na kuiita elimu ya wasomi mbumbumbu wa fikra.

Labda tujiulize, je utaratibu huu wa kusajili walimu kujiunga katika vyuo je umeleta manufaa gani? elimu yetu imetusaidia nini? na walimu wale je kweli walifeli kwa kuwa hawana akili? ama kwakuwa mitihani yao ilitungwa na walimu waliofeli na ndio maana nao kwakuwa walikuwa wana akili wakashindwa kuelewa mitihani ya walimu wao ambao hawakuwa na vigezo vya kuwa waalimu.

Taifa la leo linahitaji watu makini, waliofundishwa na walimu makini , ambao ni shahiri dhahiri kuwa katika mitihani wanapata alama za juu, lakini ni vema kuzingatia kuwa kupata alama za juu sio kigezo cha kutosha cha kumpima mwanafunzi.

Baadhi ya watu husema, kusoma kuelewa, kufaulu mtihani ni majaliwa. Kwa ufupi hakuna majaliwa yoyote kwatika kufaulu mitihani, kama unachofundishwa ndicho kinajiri katika mitihani, basi huna budi kufaulu kwa uelewa wa hali ya juu.

Kwa upande mwingine, kwakuwa walimu hawawezi kufundisha kila kitu darasani, basi maswali ya kutumia elimu dunia pia yanaweza kuzingatiwa zaidi kupima uelewa wa mwanafunzi. Kwa hali hiyo tutakuwa na taifa la watu makini wa ukweli na sio umakini wa kufundishwa na walimu wanaoitwa kuwa walifeli.

Tanzania yetu inahitaji heshima kwa waalimu wetu kwakuwa hawakufeli, bali walipimwa kwa vigezo duni. Lakini vilevile waliofeli hata siku moja hawastahili kuwa walimu wa kulikomboa taifa letu kwa kufundisha wanafunzi. Basi kwa kuwa nchi yetu kwa sasa haihitaji nadharia za kikoloni, na linahitaji watu makini, basi kama wanafunzi watapimwa vizuri, vyuo vya ualimu vipokee wanafunzi waliopata daraja la kwanza ama la pili wawe walimu na ndio hapo tutapata kizazi cha watu makini.


maoni kwa Dennis Mwasalanga

post comment chini ya makala hii, ama

0717 112 777




0 comments:

Post a Comment